Kumbukumbu La Sheria 4:19-35 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Jihadharini ili wakati mtakapoangalia na kutazama jua, mwezi na nyota na jeshi lote la mbinguni, msije mkashawishiwa kuviabudu na kuvitumikia, maana vitu hivyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliviumba kwa ajili ya watu wote duniani.

20. Lakini nyinyi ndio watu aliowakomboa kutoka Misri katika tanuri la chuma. Aliwatoeni huko ili muwe watu wake kama vile mlivyo hivi leo.

21. Kwa sababu yenu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alinikasirikia, akaapa kwamba mimi sitavuka mto Yordani kuingia katika nchi ile nzuri anayowapeni iwe mali yenu.

22. Mimi nitafia katika nchi hii wala sitauvuka mto, lakini nyinyi mko karibu kuuvuka na kwenda kuimiliki nchi ile nzuri.

23. Jihadharini sana msije mkasahau agano ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amefanya nanyi; msijifanyie sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu chochote ambacho Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewakataza kumfananisha,

24. maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni moto uteketezao; yeye ni Mungu mwenye wivu.

25. “Mtakapokuwa mmekaa katika nchi hiyo, mkapata watoto na wajukuu na kuwa wazee, kama mkianza kupotoka na kujifanyia sanamu ya kuchonga katika umbo la kitu chochote, mkafanya uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kumkasirisha,

26. basi, mimi leo naziita mbingu na dunia zishuhudie kati yenu; nawaambieni kwamba mara moja mtaangamia kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki huko ngambo ya mto Yordani. Hamtaishi huko muda mrefu, bali mtaangamizwa kabisa.

27. Mwenyezi-Mungu atawatawanya kati ya mataifa mengine, na ni wachache wenu tu watakaosalia huko ambako Mwenyezi-Mungu atawafukuzia.

28. Huko mtaitumikia miungu ya miti na mawe ambayo imetengenezwa kwa mikono ya watu; na ambayo haiwezi kuona, haisikii, haili wala kunusa.

29. Kisha kutoka humohumo nchini mtamtafuta Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtampata kama mkimtafuta kwa moyo wote na roho yote.

30. Mambo haya yote yatakapowapata huko baadaye, mkapata taabu, mtamrudia Mwenyezi-Mungu na kumtii.

31. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni Mungu mwenye rehema, hatawaacheni wala kuwaangamiza, wala kusahau agano ambalo alifanya na wazee wenu kwa kiapo.

32. “Fikirini sana juu ya matukio ya zamani, mambo yaliyotukia kabla nyinyi hamjazaliwa, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu duniani. Ulizeni ulimwenguni kote, toka pembe moja hadi nyingine, kama jambo la ajabu la namna hii limepata kutokea au kusikika!

33. Je, watu walikwisha sikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama nyinyi mlivyosikia, wakabaki hai?

34. Je, kuna Mungu yeyote mwingine aliyejaribu kamwe kwenda kujichukulia taifa lake kutoka taifa jingine, kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyofanya, kwa kutumia majaribio, ishara na maajabu, kwa vita na kwa nguvu yake kuu, akasababisha mambo ya kutisha ambayo nyinyi mlishuhudia kwa macho yenu kule Misri?

35. Nyinyi mlijaliwa kuyaona mambo hayo, ili mpate kutambua kwamba Mwenyezi-Mungu, ndiye peke yake Mungu na wala hakuna mwingine.

Kumbukumbu La Sheria 4