Kumbukumbu La Sheria 6:14-25 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Msiabudu miungu mingine, miungu ya watu walio jirani nanyi,

15. hasira ya Mwenyezi-Mungu isije ikawaka juu yenu, naye akawafutilia mbali kutoka duniani, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliye kati yenu, ni Mungu mwenye wivu.

16. “Msimjaribu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa.

17. Hakikisheni kwamba mnazitii amri zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maamuzi na masharti yake ambayo amewaamuru.

18. Fanyeni yale yanayompendeza Mwenyezi-Mungu, ili mpate kufanikiwa. Mtaweza kuimiliki nchi ile nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu aliapa kuwapa babu zenu,

19. na kwamba Mwenyezi-Mungu atawafukuza adui zenu kama alivyoahidi.

20. “Siku zijazo, watoto wenu wakiwauliza, ‘Nini maana ya maamuzi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, aliwaamuru kutenda?’

21. Nyinyi mtawajibu hivi: ‘Sisi tulikuwa watumwa wa Farao, mfalme wa Misri, na Mwenyezi-Mungu akatuokoa kwa mkono wake wenye nguvu.

22. Kwa macho yetu wenyewe tulimwona akifanya ishara na miujiza na mambo ya kutisha na ya ajabu dhidi ya Wamisri, mfalme wao na wakuu wake.

23. Alitutoa Misri, akatuleta hapa na kutupa nchi hii, kama alivyoapa kwamba atawapa babu zetu.

24. Basi, Mwenyezi-Mungu alituamuru kuzitii kanuni hizi zote na kumcha kwa faida yetu wenyewe; apate kutulinda daima kama hivi leo.

25. Tena tutakuwa waadilifu kama tukitimiza kwa uangalifu amri hizi zote mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyotuamuru’.

Kumbukumbu La Sheria 6