Kumbukumbu La Sheria 7:2-12 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Pia, baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuyatia mikononi mwenu, mkawashinda watu hao na kuwaangamiza kabisa, msifanye agano lolote nao wala msiwahurumie.

3. Msioane nao, wala msiwaoze binti zenu au wana wenu kwao.

4. Mkifanya hivyo wao watawapotosha watoto wenu wasimfuate Mwenyezi-Mungu, na kuwafanya waabudu miungu mingine, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, halafu atawaangamiza mara moja.

5. Lakini watendeni hivi: Mtazivunjilia mbali madhabahu zao na kuzibomoa nguzo zao. Na sanamu za Ashera mtazikatilia mbali na kuzitia moto sanamu zao za kuchonga.

6. Fanyeni hivyo kwa kuwa nyinyi mmewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kati ya watu wote ulimwenguni aliwachagua nyinyi ili muwe taifa lake mwenyewe.

7. “Mwenyezi-Mungu hakuwapenda nyinyi na kuwateua kwa kuwa nyinyi ni wengi mno kuliko watu wengine; nyinyi mlikuwa wachache kuliko mataifa mengine duniani.

8. Lakini ni kwa sababu Mwenyezi-Mungu anawapenda na anashika kiapo alichowaapia babu zenu, ndiyo maana aliwaokoeni kwa mkono wake wenye nguvu na kuwaokoa toka utumwani, toka mikono ya Farao mfalme wa Misri.

9. Basi, jueni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayeshika agano lake na huwaonesha fadhili kwa vizazi vingi vya wale wanaoshika amri zake.

10. Lakini huwalipa wanavyostahili wale wanaomchukia, wala hatasita kuwaadhibu wanaomchukia.

11. Kwa hiyo muwe waangalifu kushika amri, masharti na maagizo ninayowaamuru leo.

12. “Mkisikiliza maagizo haya na kuyashika hata kuyatenda, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atashika agano lake nanyi na atawaonesheni fadhili kama alivyowaahidi babu zenu.

Kumbukumbu La Sheria 7