8. Wala hakuna taifa lingine lolote hata liwe kuu namna gani, lenye masharti na maagizo ya haki, kama hayo ambayo nimewafundisha siku hii ya leo.
9. “Lakini muwe waangalifu na kujihadhari sana msije mkasahau mambo yale mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe. Isije ikatokea hata mara moja maishani mwenu mambo hayo yakasahaulika mioyoni mwenu. Wasimulieni watoto wenu na wajukuu wenu
10. juu ya siku ile ambayo mlisimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, aliponiambia, ‘Wakusanye hao watu mbele yangu, niwaambie maneno yangu ili wajifunze kunicha mimi siku zote za maisha yao, na kuwafundisha watoto wao kufanya hivyo’.
11. “Basi, mlikaribia na kusimama chini ya ule mlima ambao wakati huo ulikuwa unawaka moto uliofika mpaka mbinguni ukiwa umetanda giza na wingu zito.
12. Kisha Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi kutoka katikati ya moto huo; mliyasikia maneno aliyosema lakini hamkumwona; mlisikia tu sauti yake.
13. Naye akawatangazia agano lake akawaamuru mlishike yaani mzitii zile amri kumi ambazo aliziandika juu ya vibao viwili vya mawe.
14. Wakati huo Mwenyezi-Mungu aliniamuru niwafundishe masharti na maagizo yote ambayo mnapaswa kuyatekeleza katika nchi mnayokwenda kuimiliki.
15. “Kwa hiyo muwe waangalifu msije kusahau kwamba: Mwenyezi-Mungu alipoongea nanyi kule mlimani Horebu katikati ya moto hamkumwona kwa umbo. Kwa sababu hiyo jihadharini sana,
16. msipotoke kwa kujifanyia sanamu yoyote ya kuchonga, au ya umbo au mfano wowote, mfano wa kiume au wa kike,