Kumbukumbu La Sheria 29:20-27 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Mwenyezi-Mungu hatasamehe mtu huyo, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu na wivu wake vitamwakia mtu huyo; laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamjia, naye Mwenyezi-Mungu atalifuta kabisa jina la mtu huyo kutoka duniani.

21. Mwenyezi-Mungu atamtenga kutoka miongoni mwa makabila yote ya Israeli apatwe na maafa kufuatana na laana zote za agano zilizoandikwa katika kitabu hiki.

22. Katika vizazi vijavyo, wazawa wenu na wageni kutoka nchi ya mbali wataona jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoiletea nchi hii maafa na mateso:

23. Imejaa madini ya kiberiti na chumvi, imeteketea na kuwa tupu, haikupandwa mbegu na haioti chochote. Ni kama ilivyokuwa wakati Mwenyezi-Mungu alipoangamiza Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, kwa hasira yake kali.

24. Naam, mataifa yote yatasema: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameitendea hivyo nchi hii? Hasira hii kubwa inamaanisha nini?’

25. Na jibu litatolewa: ‘Ni kwa sababu walivunja agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao ambalo alifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri,

26. wakaenda kuitumikia na kuiabudu miungu mingine, ambayo hawakuijua hapo awali, wala Mwenyezi-Mungu hakuwa amewapa.

27. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya nchi hii, na kuiletea laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki.

Kumbukumbu La Sheria 29