Kumbukumbu La Sheria 28:31-43 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Ngombe wenu watachinjwa mbele ya macho yenu lakini hamtaonja hata kipande cha nyama yao. Punda wenu watachukuliwa kwa nguvu mbele ya macho yenu wala hamtarudishiwa. Kondoo wenu watapewa adui zenu, na hakuna mtu atakayeweza kuwasaidia.

32. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatolewa kwa watu wengine huku mkikodoa macho mchana kutwa kuwatazamia warudi, lakini hamtakuwa na nguvu ya kufanya chochote.

33. “Taifa msilolijua litachukua mazao yote ya nchi yenu na matunda ya jasho lenu, nanyi mtadhulumiwa na kuteswa daima,

34. hata mtapata wazimu kwa mambo mtakayoona kwa macho yenu wenyewe.

35. Mwenyezi-Mungu atayashambulia magoti yenu na miguu yenu kwa majipu mabaya ambayo hamtaweza kuponywa; yatawaenea tangu utosini mpaka nyayo za miguu.

36. “Mwenyezi-Mungu atawapeleka nyinyi na mfalme wenu mtakayejichagulia, mpaka kwa taifa ambalo nyinyi hamkulijua wala wazee wenu. Na huko mtatumikia miungu mingine ya miti na mawe.

37. Nanyi mtakuwa kinyaa, dharau na mshangao miongoni mwa watu wote wa nchi ambako Mwenyezi-Mungu atawapeleka.

38. Mtapanda mbegu nyingi lakini mtavuna kidogo tu kwa kuwa nzige watakula mazao yenu.

39. Mtapanda mizabibu na kuitunza, lakini hamtavuna mizabibu hiyo wala kunywa divai yake, maana wadudu wataila.

40. Mtakuwa na mizeituni mahali pote nchini mwenu, lakini hamtakuwa na mafuta ya kujipaka; kwa sababu zeituni hizo zitapukutika.

41. Mtazaa watoto wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wenu, watachukuliwa uhamishoni.

42. Matunda yenu yote na mazao yenu mashambani vitamilikiwa na nzige.

43. “Wageni waishio katika nchi yenu watazidi kupata nguvu huku nyinyi mkizidi kufifia zaidi na zaidi.

Kumbukumbu La Sheria 28