Kumbukumbu La Sheria 26:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Kisha tukamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wetu, akasikia kilio chetu, na kuyaona mateso yetu, kazi ngumu na dhuluma tulizozipata.

8. Basi, Mwenyezi-Mungu akatutoa huko Misri kwa mkono wake wa nguvu ulionyoshwa, kwa vitisho, ishara na maajabu.

9. Alituleta hapa na kutupatia nchi hii inayotiririka maziwa na asali.

10. Na sasa ninamletea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya mazao ya nchi ambayo amenipa.’“Kisha utaweka kikapu chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuabudu mbele zake.

11. Nawe utafurahia mema yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amekujalia wewe na jamaa yako. Nao watafurahi pamoja nawe.

12. Kila baada ya miaka mitatu, kila mmoja wenu atatoa sehemu moja ya kumi ya mazao yake yote kwa ajili ya Walawi na wageni, yatima na wajane, ili wapate chakula chote wanachohitaji wanapokuwa katika miji yenu.

13. Kisha utasema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, hivi: ‘Nimelitoa nyumbani kwangu fungu takatifu, nikawapa Walawi, wageni, yatima na wajane, kama ulivyoniamuru nifanye. Sijavunja amri zako wala sijasahau.

14. Sikula zaka yoyote nilipokuwa ninaomboleza; sikuitoa nje ya nyumba yangu nilipokuwa najisi na sikutoa zaka hiyo kwa wafu. Nimekutii ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoamuru.

15. Uangalie chini kutoka makao yako matakatifu mbinguni, uwabariki watu wako Israeli na nchi uliyotupatia kama ulivyowaapia wazee wetu; nchi inayotiririka maziwa na asali.’

16. “Leo hii, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaamuru kuyashika masharti na maagizo haya. Muwe waangalifu kuyatekeleza kwa moyo wote na roho yote.

17. Leo hii mmekiri Mwenyezi-Mungu, kuwa Mungu wenu, na kwamba mtafuata njia zake na kushika masharti, amri zake na maagizo yake na kutii sauti yake.

18. Naye Mwenyezi-Mungu ametamka rasmi leo hii kwamba nyinyi ni watu wake yeye mwenyewe kama alivyowaahidi na kwamba mnatakiwa kushika amri zake zote.

Kumbukumbu La Sheria 26