Kumbukumbu La Sheria 24:6-15 Biblia Habari Njema (BHN)

6. “Mtu yeyote asichukue jiwe la chini au la juu la kusagia kuwa rehani; kufanya hivyo ni kama kuchukua uhai wa mtu huyo.

7. “Mtu yeyote akimwiba Mwisraeli mwenzake na kumfanya mtumwa wake au kumwuza utumwani, mtu huyo lazima auawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.

8. “Kama mtu akishikwa na ukoma mnapaswa kuwa waangalifu kufuata maagizo ya Walawi. Kama nilivyowaamuru ndivyo mtakavyofuata kwa uangalifu.

9. Kumbukeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu alivyomtendea Miriamu mlipokuwa safarini kutoka Misri.

10. “Ukimkopesha jirani kitu chochote, usiingie kwake kuchukua rehani.

11. Msubiri nje na umwache yeye mwenyewe akuletee hiyo rehani.

12. Kama yeye ni maskini usikae na rehani hiyo usiku kucha.

13. Mrudishie kila siku jioni ili usiku aweze kujifunika na kukutakia baraka. Kufanya hivyo ni jambo la uadilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

14. “Usimdhulumu kibarua maskini na mhitaji, awe Mwisraeli au mmoja wa wageni wanaoishi katika miji yenu.

15. Kila siku, kabla jua halijakuchwa, mlipe ujira wake wa siku hiyo, maana yeye ni maskini na huo ujira ni tegemeo la moyo wake; ili asije akamlilia Mwenyezi-Mungu, nawe ukawa na hatia.

Kumbukumbu La Sheria 24