Ufunuo 16:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu duniani.”

2. Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi. Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na alama ya yule mnyama na wale walioiabudu sanamu yake.

3. Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini vikafa.

4. Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, navyo vikageuka damu.

5. Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema,“Ewe mtakatifu, uliyeko na uliyekuwako!Wewe umetenda sawa kuhukumu mambo hayo.

6. Maana waliimwaga damu ya watu wa Mungu na manabii,nawe umewapa damu wainywe;wamestahili hivyo!”

7. Kisha, nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu Mwenye Nguvu! Hukumu zako ni za kweli na haki!”

8. Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake.

9. Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na uwezo juu ya mabaa hayo. Lakini hawakutubu na kumtukuza Mungu.

10. Kisha, malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu,

11. wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na madonda yao. Lakini hawakutubu matendo yao mabaya.

Ufunuo 16