8. Lakini ni kwa sababu Mwenyezi-Mungu anawapenda na anashika kiapo alichowaapia babu zenu, ndiyo maana aliwaokoeni kwa mkono wake wenye nguvu na kuwaokoa toka utumwani, toka mikono ya Farao mfalme wa Misri.
9. Basi, jueni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayeshika agano lake na huwaonesha fadhili kwa vizazi vingi vya wale wanaoshika amri zake.
10. Lakini huwalipa wanavyostahili wale wanaomchukia, wala hatasita kuwaadhibu wanaomchukia.
11. Kwa hiyo muwe waangalifu kushika amri, masharti na maagizo ninayowaamuru leo.
12. “Mkisikiliza maagizo haya na kuyashika hata kuyatenda, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atashika agano lake nanyi na atawaonesheni fadhili kama alivyowaahidi babu zenu.
13. Atawapenda na kuwabariki, nanyi mtaongezeka na kuwa na wazawa wengi; atayabariki mashamba yenu ili mpate nafaka, divai na mafuta; atawabariki kwa kuwapeni ng'ombe na kondoo wengi katika nchi aliyowaahidi babu zenu kuwa atawapeni nyinyi.
14. Mtabarikiwa kuliko watu wengine wote ulimwenguni. Miongoni mwenu hakutakuwa na mwanamume wala mwanamke tasa.
15. Mwenyezi-Mungu atawaondoleeni magonjwa yote na hamtapatwa na magonjwa yoyote ya kutisha kama yaliyowapata huko Misri, lakini atawapa maadui zenu magonjwa hayo.
16. Angamizeni taifa lolote ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; atalitia mikononi mwenu, wala msilionee huruma. Msiabudu miungu yao, kwani jambo hili litakuwa mtego kwenu.
17. “Msijisemee mioyoni mwenu: ‘Watu hawa ni wengi kuliko sisi, twawezaje kuwafukuza nchini?’
18. Msiwaogope, kumbukeni vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyomtendea Farao na nchi nzima ya Misri.