Kumbukumbu La Sheria 28:49-65 Biblia Habari Njema (BHN)

49. “Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi.

50. Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana;

51. litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize.

52. Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni.

53. Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni.

54. Hata mtu mpole kabisa na aliyelelewa vizuri sana atamnyima chakula ndugu yake, mkewe ampendaye na mtoto wake atakayesalia;

55. wala hatamgawia hata mmoja wao nyama ya watoto wake atakaowala. Hamtabakiwa na chochote wakati huo wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui katika miji yenu yote.

56. Hata mwanamke yule ambaye ni mpole sana na aliyelelewa vizuri na mwororo hata hajawahi kukanyaga udongo kwa kisigino chake hataweza kufanya vingine. Wakati huo wa kuzingirwa kutakuwa na njaa hata

57. atamla mtoto wake mchanga na kile kinachotoka baada ya kuzaliwa mtoto bila hata mumewe mpenzi au mmoja wa watoto wake kutambua.

58. “Kama msipokuwa waangalifu kutekeleza maneno yote ya sheria hii iliyoandikwa katika kitabu hiki na msipoliheshimu na kulitukuza jina tukufu la kuogofya la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,

59. basi, Mwenyezi-Mungu atawaleteeni nyinyi na wazawa wenu mateso yasiyo ya kawaida, mateso makali yasiyoponyeka na ya kudumu, na magonjwa makali ya kudumu.

60. Atawaleteeni tena yale magonjwa mliyoyaogopa nchini Misri, nayo yatawaandama daima.

61. Atawaleteeni magonjwa ya kila aina na mateso mengine ambayo hayakutajwa katika kitabu hiki cha sheria mpaka muangamie.

62. Ijapokuwa nyinyi ni wengi kama nyota za mbinguni, lakini mtakuwa wachache tu kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

63. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyopendezwa kuwafanikisha na kuwafanya kuwa wengi, vivyo hivyo Mwenyezi-Mungu atapendezwa kuwaletea maafa na kuwaangamiza. Nanyi mtaondolewa katika nchi hiyo ambayo mnakwenda kuimiliki.

64. Mwenyezi-Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka pembe moja ya dunia hadi nyingine na huko mtaitumikia miungu mingine ya miti na mawe, miungu ambayo nyinyi wala wazee wenu hawakuijua.

65. Hamtakuwa na raha yoyote mahali penu wenyewe pa kutulia wala miongoni mwa mataifa hayo. Ila Mwenyezi-Mungu atawapeni huko wasiwasi wa moyo, kufifia kwa macho na mahangaiko ya rohoni.

Kumbukumbu La Sheria 28