Kumbukumbu La Sheria 26:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Baada ya kufika na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapa iwe yenu na kuishi huko,

2. baadhi ya malimbuko ya mazao utakayovuna katika nchi anayokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, utayachukua katika kikapu mpaka pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amepachagua pawe makao yake.

3. Utamwendea kuhani anayehudumu wakati huo, na kumwambia, ‘Leo ninakiri mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuwa nimeingia katika nchi aliyowaapia wazee wetu kuwa atatupa.’

4. “Naye kuhani atakapochukua kikapu hicho mikononi mwako na kukiweka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,

5. utatamka maneno haya mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako: ‘Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyetangatanga huko na huko, kisha akashuka kwenda Misri akaishi huko kama mgeni. Yeye na jamaa yake walikuwa watu wachache tu walipokuwa huko, lakini wakawa taifa kubwa lenye nguvu na watu wengi.

6. Wamisri walitutendea kwa ukatili wakatutesa na kutulazimisha kufanya kazi ngumu ya watumwa.

7. Kisha tukamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wetu, akasikia kilio chetu, na kuyaona mateso yetu, kazi ngumu na dhuluma tulizozipata.

8. Basi, Mwenyezi-Mungu akatutoa huko Misri kwa mkono wake wa nguvu ulionyoshwa, kwa vitisho, ishara na maajabu.

9. Alituleta hapa na kutupatia nchi hii inayotiririka maziwa na asali.

10. Na sasa ninamletea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya mazao ya nchi ambayo amenipa.’“Kisha utaweka kikapu chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuabudu mbele zake.

11. Nawe utafurahia mema yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amekujalia wewe na jamaa yako. Nao watafurahi pamoja nawe.

12. Kila baada ya miaka mitatu, kila mmoja wenu atatoa sehemu moja ya kumi ya mazao yake yote kwa ajili ya Walawi na wageni, yatima na wajane, ili wapate chakula chote wanachohitaji wanapokuwa katika miji yenu.

13. Kisha utasema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, hivi: ‘Nimelitoa nyumbani kwangu fungu takatifu, nikawapa Walawi, wageni, yatima na wajane, kama ulivyoniamuru nifanye. Sijavunja amri zako wala sijasahau.

Kumbukumbu La Sheria 26