Kumbukumbu La Sheria 20:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Mkienda vitani kupigana na adui zenu, mkaona farasi, magari na jeshi kubwa zaidi kuliko lenu msiwaogope. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyewatoa Misri, atakuwa nanyi.

2. Kabla ya kuanza mapigano, kuhani atajitokeza mbele na kuwaambia watu,

3. ‘Watu wa Israeli sikilizeni! Leo mnakaribia kupigana dhidi ya adui zenu. Msife moyo, au kuogopa, au kutishika, au kuwaogopa adui;

4. maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayekwenda pamoja nanyi kupigana kwa niaba yenu dhidi ya adui zenu na kuwapa ushindi.’

5. “Kisha maofisa watawaambia watu: ‘Kuna mtu yeyote hapa aliyejenga nyumba mpya lakini hajaizindua? Arudi nyumbani, asije akafia vitani na mtu mwingine akaizindua.

6. Kuna mtu yeyote hapa aliyepanda mizabibu na ambaye hajafurahia matunda yake ya kwanza? Arudi nyumbani asije akafia vitani na mtu mwingine akafurahia matunda yake.

7. Kuna mwanamume yeyote hapa aliyeposa na yuko karibu kuoa? Arudi nyumbani, asije akafia vitani, na mwanamume mwingine akaoa mchumba wake.’

8. Maofisa wataendelea kuwaambia watu, ‘Je, yupo hapa mtu aliyekufa moyo? Arudi nyumbani, asije akasababisha wenzake kufa moyo kama yeye.’

9. Maofisa wakisha sema na watu, basi makamanda watawaongoza watu.

Kumbukumbu La Sheria 20