8. Mtu atakayemteketeza ng'ombe huyo pia atazifua nguo zake kwa maji na kuoga mwili kwa maji, lakini naye pia atakuwa najisi hadi jioni.
9. Mtu aliye safi atayazoa majivu ya ng'ombe huyo na kuyapeleka mahali safi nje ya kambi. Yatahifadhiwa na kutumiwa na jumuiya nzima ya Israeli kutengeneza maji ya kuondoa najisi, ili kuondoa dhambi.
10. Mtu atakayeyazoa majivu ya ng'ombe huyo lazima azifue nguo zake, lakini atakuwa najisi hadi jioni. Sharti hili ni la kudumu, na litawahusu Waisraeli na watu wengine watakaoishi pamoja nao.
11. “Mtu akigusa maiti ya mtu yeyote, atakuwa najisi kwa siku saba.
12. Siku ya tatu na ya saba mtu huyo atajiosha kwa yale maji ya utakaso, naye atakuwa safi. Lakini akiacha kujitakasa katika siku ya tatu na ya saba, mtu huyo atabaki kuwa najisi.
13. Agusaye maiti, yaani mwili wa mtu aliyekufa, asipojitakasa, analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu, naye atatengwa na wana wa Israeli. Mtu huyo atabaki najisi kwa sababu hakunyunyiziwa yale maji ya utakaso.
14. “Na hii ndiyo sheria ya kufuatwa kama mtu akifia hemani: Kila mtu atakayeingia ndani ya hema hilo, au aliye ndani ya hema hilo, atakuwa najisi kwa siku saba.