Waamuzi 20:32-48 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Watu wa Benyamini wakafikiri, “Tumewapiga kama nyakati zilizopita.” Lakini Waisraeli wakasema, “Sisi tukimbie ili tuwavute mbali na mji hadi kwenye njia kuu.”

33. Hivyo watu wote wa Israeli wakatoka kwenye sehemu yao na kujipanga tena huko Baal-tamari. Wenzao waliokuwa wanaotea wakatoka haraka mahali pao upande wa magharibi wa mji wa Gibea.

34. Askari hodari waliochaguliwa kutoka makabila yote ya Israeli wakawasili hapo mbele ya mji wa Gibea. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Lakini watu wa Benyamini hawakufahamu kwamba kuangamia kwao kulikuwa karibu.

35. Mwenyezi-Mungu aliwashinda watu wa Benyamini mbele ya Waisraeli. Waisraeli wakawaua watu wa Benyamini 25,100. Hao wote waliouawa walikuwa askari walioweza kutumia silaha.

36. Hivyo watu wa kabila la Benyamini wakaona kwamba wameshindwa.Waisraeli walirudi nyuma kana kwamba wanawakimbia watu wa kabila la Benyamini, kwani walitegemea wenzao waliokuwa wamewekwa kuotea mji wa Gibea.

37. Wale waliowekwa kuuotea mji walitoka haraka na kuushambulia mji wa Gibea na kuwaua wote waliokuwamo kwa upanga.

38. Walikuwa wamekubaliana na wale watu wengine wa Israeli juu ya ishara moja. Walikubaliana kwamba wale waliokuwa wanaotea watakapoona moshi mkubwa unapanda juu kutoka mjini,

39. basi, waushambulie mji. Wakati huo, watu wa kabila la Benyamini walikuwa tayari wameua watu wapatao thelathini wa Israeli na kuambiana, “Tumewapiga kama hapo awali.”

40. Lakini ile ishara ya mnara wa moshi ilipoanza kutokea katika mji, watu wa kabila la Benyamini walipotazama nyuma yao, wakashangaa kuona kwamba mji wao ulikuwa unateketezwa moto.

41. Ndipo Waisraeli wakageuka, na watu wa kabila la Benyamini wakakumbwa na fadhaa kwani sasa waliona kuwa kuangamia kwao kulikuwa kumekaribia.

42. Kwa hiyo wakageuka, wakawakimbia Waisraeli kuelekea jangwani, lakini vita vikawakumba; wakajikuta wako katikati ya majeshi mawili ya Israeli, na askari waliotoka wakawaangamiza.

43. Waisraeli waliwazingira watu wa kabila la Benyamini, wakawafuatia kutoka Noha hadi mashariki ya mji wa Gibea wakiwaua wengi wao.

44. Siku hiyo watu 18,000 wa kabila la Benyamini, wote askari hodari, waliuawa.

45. Watu wengine wa kabila la Benyamini waligeuka, wakakimbia kuelekea jangwani hadi mwamba wa Rimoni. Wengine 5,000 waliuawa kwenye njia kuu walipokuwa wanakimbia. Waisraeli waliendelea kuwafuatia vikali watu wa kabila la Benyamini hadi mji wa Gidomu wakawaua watu 2,000.

46. Jumla ya watu wote wa kabila la Benyamini waliouawa siku hiyo ilikuwa 25,000, askari hodari wa kutumia silaha.

47. Lakini wanaume 600 wa kabila la Benyamini walifaulu kukimbilia jangwani hadi kwenye mwamba wa Rimoni, wakakaa huko kwa muda wa miezi minne.

48. Waisraeli wakawageukia watu wengine wa kabila la Benyamini, wakawaua wote: Wanaume, wanawake, watoto na wanyama. Na miji yote waliyoikuta huko wakaiteketeza moto.

Waamuzi 20