Kumbukumbu La Sheria 3:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Kisha, tuligeuka, tukapanda kuelekea Bashani. Mfalme Ogu alitoka na watu wake wote kupigana nasi karibu na mji wa Edrei.

2. Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Usimwogope, maana nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake na nchi yake. Utamtendea kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori aliyekaa kule Heshboni’.

3. “Basi, Mwenyezi-Mungu alimtia mikononi mwetu mfalme Ogu wa Bashani na watu wake, tukawaangamiza hata asibakie mtu yeyote.

4. Tuliiteka miji yake yote; hakuna hata mji mmoja ambao hatukuuteka. Jumla tuliiteka miji sitini, yaani eneo lote la Argobu ambalo lilitawaliwa na mfalme Ogu wa Bashani.

5. Miji yote hii ilikuwa na ngome zenye kuta ndefu, zilizokuwa na malango na makomeo. Kulikuwa pia na vijiji vingi ambavyo havikuzungukwa na kuta.

6. Tuliteketeza kila kitu huko, tukaharibu kila mji na kuua wanaume, wanawake na watoto kama tulivyofanya katika miji ya mfalme Sihoni wa Heshboni.

7. Lakini mifugo yote na mali tulichukua nyara.

8. “Wakati huo tuliitwaa nchi hiyo ya wale wafalme wawili wa Waamori waliokuwa wanakaa ngambo ya mto Yordani, katikati ya mto Arnoni na mlima Hermoni.

9. (Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri).

Kumbukumbu La Sheria 3