Kumbukumbu La Sheria 28:41-53 Biblia Habari Njema (BHN)

41. Mtazaa watoto wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wenu, watachukuliwa uhamishoni.

42. Matunda yenu yote na mazao yenu mashambani vitamilikiwa na nzige.

43. “Wageni waishio katika nchi yenu watazidi kupata nguvu huku nyinyi mkizidi kufifia zaidi na zaidi.

44. Wao watawakopesha nyinyi, lakini nyinyi hamtakuwa na uwezo wa kuwakopesha. Wao watakuwa wa kwanza kwa nguvu nanyi mtakuwa wa mwisho.

45. “Hayo yote yatawapateni nyinyi na kuwaandama mpaka muangamizwe kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kuhusu kushika amri zake na masharti aliyowapa.

46. Lakini hizo zitakuwa ushahidi wa hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwenu na wazawa wenu milele.

47. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwabariki katika kila njia, lakini nyinyi hamkumtumikia kwa moyo wa furaha na mkunjufu.

48. Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize.

49. “Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi.

50. Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana;

51. litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize.

52. Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni.

53. Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni.

Kumbukumbu La Sheria 28