Kumbukumbu La Sheria 28:21-32 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Atawaleteeni maradhi mabaya mpaka wote muangamie kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki.

22. Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa kifua kikuu, homa, majipu, joto kali, ukame, dhoruba na ukungu; mambo hayo yatawaandama mpaka mmeangamia.

23. Mbingu zitakauka kama shaba nyeusi bila mvua, na nchi itakuwa kama chuma.

24. Mwenyezi-Mungu ataifanya vumbi na mchanga kuwa mvua yenu, vumbi litawanyeshea mpaka mmeangamizwa.

25. “Mwenyezi-Mungu atawafanya mshindwe na adui zenu. Nyinyi mtakwenda kuwakabili kwa njia moja, lakini mtawakimbia kwa njia saba. Nanyi mtakuwa kinyaa kwa watu wote duniani.

26. Maiti zenu zitakuwa chakula cha ndege wala hapatakuwa na mtu atakayewafukuza.

27. Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa majipu yaliyowapata Wamisri, atawapeni vidonda, upele na kuwashwa ambavyo hamwezi kuponywa.

28. Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa pigo la kuwa na wazimu, mtakuwa vipofu na kuvurugika akili.

29. Mtakwenda kwa kupapasapapasa mchana kama vipofu wala hamtafanikiwa katika shughuli zenu. Mtakuwa mkidhulumiwa kila mara na hakutakuwa na mtu wa kuwasaidieni.

30. “Mtachumbia wasichana lakini watu wengine watalala nao. Mkijenga nyumba watu wengine watakaa ndani yake. Mkipanda mizabibu watu wengine watavuna.

31. Ngombe wenu watachinjwa mbele ya macho yenu lakini hamtaonja hata kipande cha nyama yao. Punda wenu watachukuliwa kwa nguvu mbele ya macho yenu wala hamtarudishiwa. Kondoo wenu watapewa adui zenu, na hakuna mtu atakayeweza kuwasaidia.

32. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatolewa kwa watu wengine huku mkikodoa macho mchana kutwa kuwatazamia warudi, lakini hamtakuwa na nguvu ya kufanya chochote.

Kumbukumbu La Sheria 28