17. Vikapu vyenu vya nafaka vitalaaniwa na vyombo vyenu vya kukandia mkate.
18. Watoto wenu watalaaniwa na mazao yenu ya nchi; mifugo yenu italaaniwa isiongezeke.
19. Mtalaaniwa mnapoingia na mnapotoka.
20. “Mwenyezi-Mungu atawaleteeni maafa, vurugu na kukata tamaa katika shughuli zenu zote mpaka mmeangamia upesi kwa sababu ya uovu wa matendo yenu na kwa sababu ya kumwacha Mwenyezi-Mungu.
21. Atawaleteeni maradhi mabaya mpaka wote muangamie kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki.
22. Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa kifua kikuu, homa, majipu, joto kali, ukame, dhoruba na ukungu; mambo hayo yatawaandama mpaka mmeangamia.
23. Mbingu zitakauka kama shaba nyeusi bila mvua, na nchi itakuwa kama chuma.
24. Mwenyezi-Mungu ataifanya vumbi na mchanga kuwa mvua yenu, vumbi litawanyeshea mpaka mmeangamizwa.