Kumbukumbu La Sheria 22:18-30 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Hapo wazee wa mji watamchukua yule mwanamume na kumpiga viboko.

19. Pia watamtoza mtu huyo faini ya vipande 100 vya fedha na kupewa baba wa huyo mwanamke kwa kuwa mwanamume huyo amemharibia sifa binti wa Israeli. Na huyo mwanamke ataendelea kuwa mke wake na hataweza kumpa talaka maisha yake yote.

20. Lakini kama mashtaka hayo ni ya kweli, na hakuna ushahidi wa ubikira wake,

21. watampeleka kwenye mlango wa nyumba ya baba yake na wanaume wa mji huo watampiga mawe afe, kwa sababu amefanya ufidhuli katika Israeli kwa kufanya umalaya akiwa nyumbani kwa baba yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu.

22. “Mwanamume akifumaniwa na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanamume na mwanamke, lazima wauawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu.

23. “Mwanamume akimkuta msichana aliyechumbiwa, akalala naye,

24. mtawatoa wote wawili nje ya mji na kuwapiga mawe mpaka wafe. Msichana huyo lazima auawe kwa kuwa hakupiga kelele asaidiwe ingawa alikuwa mjini; naye mwanamume lazima auawe kwa kuwa amemchafua mchumba wa jirani yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu.

25. “Lakini kama mwanamume amekutana na msichana aliyechumbiwa akamshika kwa nguvu, basi ni huyo mwanamume tu atakayeuawa.

26. Msimtendee huyo msichana chochote; yeye hana kosa linalostahili adhabu ya kifo. Tukio hili ni sawa na la mtu anayemshambulia mtu mwingine na kumwua, kwa sababu

27. mwanamume huyo alimshika kwa nguvu huyo msichana huko mbugani, na ingawa alipiga kelele kuomba msaada hapakuwa na mtu wa kumsaidia.

28. “Mwanamume akikutana na msichana ambaye hajachumbiwa, akamshika kwa nguvu, wakafumaniwa,

29. mwanamume huyo atamlipa baba yake msichana huyo vipande hamsini vya fedha kwa sababu amemnajisi, na msichana huyo atakuwa mke wake, wala hana ruhusa ya kumwacha maisha yake yote.

30. “Mwanamume yeyote kamwe asilale na mke wa baba yake.

Kumbukumbu La Sheria 22