Kumbukumbu La Sheria 16:3-10 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Msile sadaka hiyo na mikate iliyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso – kwa sababu mlitoka Misri kwa haraka; kwa hiyo, muda wote mtakaoishi mtakumbuka ile siku mlipotoka Misri.

4. Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi.

5. Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa,

6. bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri.

7. Hiyo nyama mtaichemsha na kuila mahali pale Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakapochagua; asubuhi yake mtageuka na kurudi mahemani mwenu.

8. Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu; na mnamo siku ya saba utakuwapo mkutano mkubwa wa kumwabudu Mwenyezi-Mungu, na msifanye kazi yoyote siku hiyo.

9. “Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka.

10. Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Kumbukumbu La Sheria 16