Kumbukumbu La Sheria 11:24-32 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; nchi yenu itaenea kutoka jangwani, upande wa kusini, hadi milima ya Lebanoni upande wa kaskazini, na kutoka mto Eufrate upande wa mashariki, hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi.

25. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwakabili. Popote mtakapokwenda katika nchi hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatia watu hofu wawaogope, kama alivyowaahidi.

26. “Angalieni, leo hii nawawekea mbele yenu baraka na laana:

27. Baraka, kama mtatii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo nawapeni hivi leo;

28. na laana, kama hamtazitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuiacha njia ninayowaamuru, mkaabudu miungu mingine ambayo hata hamjawahi kuijua.

29. Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha kwenye nchi mnayokwenda kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka mlima Gerizimu, na laana kutoka mlima Ebali.

30. (Milima hii iko ngambo ya mto Yordani, magharibi ya barabara kuelekea machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waishio Araba mkabala wa Gilgali).

31. Itawabidi kuvuka mto Yordani mwingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni. Basi, mtakapoimiliki na kukaa humo,

32. muwe waangalifu kutimiza masharti yote na maagizo ninayowapa leo.

Kumbukumbu La Sheria 11