18. “Yawekeni maneno yangu haya mioyoni mwenu na rohoni mwenu. Yafungeni mikononi mwenu kama alama na kuyavaa katika paji la uso.
19. Wafundisheni watoto wenu maneno haya mkiyazungumzia mketipo katika nyumba zenu, mnapotembea, mnapolala na mnapoamka.
20. Ziandikeni katika vizingiti vya nyumba zenu, na katika malango yenu,
21. ili nyinyi na watoto wenu mpate kuishi maisha marefu katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliapa kuwapa babu zenu, siku zote mbingu zitakapodumu juu ya dunia.
22. “Mkijihadhari kutenda amri zote ambazo nimewapa: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote na kuambatana naye,
23. basi Mwenyezi-Mungu atayafukuza mataifa yote hayo mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi iliyo mali ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi.
24. Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; nchi yenu itaenea kutoka jangwani, upande wa kusini, hadi milima ya Lebanoni upande wa kaskazini, na kutoka mto Eufrate upande wa mashariki, hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi.