Kumbukumbu La Sheria 1:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kitabu hiki kina maneno ambayo Mose aliwaambia watu wote wa Israeli wakati walipokuwa nyikani mashariki ya mto Yordani. Walikuwa katika bonde la Yordani karibu na Sufu, kati ya mji wa Parani upande mmoja na mji wa Tofeli, Labani, Hazerothi na Dizahabu, upande mwingine.

2. (Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka mlima Horebu hadi Kadesh-barnea kwa njia ya mlima Seiri.)

3. Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, mwaka wa arubaini, baada ya kutoka Misri, Mose aliwaambia watu kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru awaambie.

4. Alifanya hivyo baada ya kumshinda mfalme Sihoni wa Waamori ambaye alikuwa anakaa mjini Heshboni, na mfalme Ogu wa Bashani ambaye alikuwa anakaa mjini Ashtarothi na Edrei.

5. Mose alichukua jukumu la kuwaelezea watu sheria ya Mungu wakati walipokuwa ngambo ya pili ya mto Yordani.Aliwaambia hivi:

6. “Tulipokuwa mlimani Sinai, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu alituambia hivi: ‘Mmekaa muda wa kutosha kwenye mlima huu;

7. sasa vunjeni kambi yenu mwendelee na safari. Nendeni kwenye nchi ya milima ya Waamori na maeneo ya nchi jirani katika Araba, kwenye milima na mabonde, huko Negebu na sehemu za pwani; naam, nendeni mpaka nchi ya Kanaani, na nchi ya Lebanoni, hadi kwenye ule mto mkubwa wa Eufrate.

8. Nchi hii yote nimeiweka mbele yenu. Basi, nendeni mkaimiliki nchi hiyo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu niliapa kuwapa wazee wenu Abrahamu, Isaka, Yakobo na wazawa wao.’”

9. Mose akawaambia watu, “Tulipokuwa bado mlimani Sinai, mimi niliwaambieni hivi: ‘Jukumu la kuwaongozeni ni kubwa mno kwangu mimi peke yangu.

10. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya muwe wengi; leo mmekuwa wengi kama nyota za mbinguni.

11. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na awafanye mzidi kuongezeka mara elfu zaidi ya mlivyo sasa na kuwabariki kama alivyoahidi!

12. Lakini mimi peke yangu nitawezaje kuchukua jukumu hilo zito la kusuluhisha ugomvi wenu?

13. Chagueni kutoka katika kila kabila watu wenye hekima, busara na ujuzi ili niwateue wawe viongozi wenu.’

14. Nyinyi mlikubali, mkanijibu hivi: ‘Jambo ulilosema ni la busara’.

15. Hivyo niliwachukua wale viongozi wenye hekima, busara na ujuzi ambao mliwachagua kutoka katika makabila yenu, nikawaweka kuwa viongozi wenu. Niliwaweka wengine kuwa makamanda wa makundi ya watu elfuelfu, ya watu miamia, ya watu hamsinihamsini na ya watu kumikumi. Nilichagua pia maofisa wengine wa kuchunga kila kabila.

16. “Wakati huohuo niliwapa waamuzi wenu maagizo yafuatayo: ‘Sikilizeni kesi za watu wenu. Toeni hukumu za haki katika visa vya watu wenu, kadhalika na mizozo ya wageni waishio pamoja nanyi.

17. Msimpendelee mtu yeyote katika kutoa hukumu; mtawasikiliza bila upendeleo, wakubwa kwa wadogo. Msitishwe na mtu yeyote, maana hukumu mnayotoa inatoka kwa Mungu. Kesi yoyote ikiwa ngumu zaidi kwenu, ileteni kwangu, nami nitaisikiliza.’

Kumbukumbu La Sheria 1