Hesabu 10:10-27 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Hali kadhalika katika siku zenu za furaha, kama vile sikukuu za mwandamo wa mwezi na sikukuu nyinginezo, mtazipiga tarumbeta hizi wakati mnapotoa sadaka zenu za kuteketezwa na tambiko za sadaka zenu za amani. Hapo mimi Mungu wenu nitawakumbukeni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

11. Mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu wana wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la maamuzi liliinuliwa,

12. nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo lilipaa na hatimaye likatua katika jangwa la Parani.

13. Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama ilivyotolewa na Mose.

14. Wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi cha kabila la Yuda, walitangulia, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu.

15. Nethaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Isakari.

16. Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Zebuluni.

17. Kisha, hema lilishushwa, na watu wa ukoo wa Gershoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka.

18. Halafu, watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Reubeni, walifuata kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.

19. Shelumieli mwana wa Suri-shadai, aliliongoza kabila la Simeoni.

20. Naye Eliasafu mwana wa Deueli, aliliongoza kabila la Gadi.

21. Kisha walifuata watu wa ukoo wa Kohathi, wakiwa wamebeba vyombo vitakatifu. Walipowasili, hema lilikuwa limekwisha simikwa.

22. Baada ya hao, walifuata watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Efraimu, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elishama mwana wa Amihudi.

23. Gamalieli mwana wa Pedasuri aliliongoza kabila la Manase,

24. naye Abidani mwana wa Gideoni, aliliongoza kabila la Benyamini.

25. Mwisho, wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Dani, waliokuwa kama walinzi nyuma ya vikosi vyote, walisafiri, kundi moja baada ya jingine. Hawa waliongozwa na Ahiezeri mwana wa Amishadai.

26. Pagieli, mwana wa Okrani, aliliongoza kabila la Asheri.

27. Naye Ahira mwana wa Enani, aliliongoza kabila la Naftali.

Hesabu 10