1 Samueli 14:2-21 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Shauli alikuwa amepiga kambi chini ya mkomamanga huko Migroni, nje ya mji wa Gibea, akiwa pamoja na watu wapatao 600.

3. Ahiya, mwana wa Ahitubu ndugu yake Ikabodi mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi-Mungu mjini Shilo, alikuwa ndiye aliyevaa kizibao cha kuhani. Watu hawakujua kwamba Yonathani amekwisha ondoka.

4. Kwenye kipito ambako Yonathani alipaswa apitie ili afike kwenye ngome ya Wafilisti, kulikuwa na miamba miwili iliyochongoka, upande huu na upande mwingine. Mwamba mmoja uliitwa Bosesi na mwingine uliitwa Sene.

5. Mwamba mmoja ulikuwa kaskazini mwa mji wa Mikmashi na mwingine ulikuwa kusini mkabala na mji wa Gibea.

6. Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende upande wa pili kwenye ile ngome ya hawa watu wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi-Mungu akatusaidia, maana Mwenyezi-Mungu haokoi kwa kutegemea wingi au uchache wa watu.”

7. Yule kijana aliyembebea silaha akamwambia, “Fanya chochote unachotaka kufanya, mimi niko pamoja nawe kwani wazo lako ndilo wazo langu.”

8. Yonathani akamwambia, “Tutavuka kuwaendea wale watu ili wapate kutuona.

9. Kama wakituambia tuwangoje, hadi waje hapa tulipo basi, tutasimama papa hapa na wala hatutawaendea.

10. Lakini wakisema sisi tuwaendee, basi tutawaendea kwani hiyo itakuwa ni ishara kuwa Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwetu.”

11. Basi, wakajitokeza ili Wafilisti wawaone. Wafilisti walipowaona wakasema, “Angalieni wale Waebrania wanatoka kwenye mashimo walimokuwa wamejificha.”

12. Wafilisti waliokuwa kwenye ngome wakamwita Yonathani na kijana aliyembebea silaha, “Njoni huku kwetu, nasi tutawaonesha kitu.”Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Nifuate; Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.”

13. Basi, Yonathani akapanda kwa miguu na mikono, na yule kijana akamfuata. Yonathani aliwashambulia Wafilisti akiwaangusha chini huku yule kijana alifuata nyuma akiwaua.

14. Katika mashambulizi hayo ya kwanza Yonathani, akiwa pamoja na kijana wake aliyembebea silaha, aliwaua watu kama ishirini katika eneo la nchi lipatalo nusu eka.

15. Katika nchi nzima ya Wafilisti, wote walianza kufadhaika, wanajeshi kambini, watu mashambani, kwenye ngome, hata na washambuliaji walitetemeka; nchi ilitetemeka, na kulikuwa na woga mkubwa.

16. Wapelelezi wa Shauli huko Gibea katika nchi ya Benyamini waliwaona watu wengi wakikimbia huku na huko.

17. Shauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, “Hebu jihesabuni ili kujua ni akina nani waliotutoroka.” Walipojihesabu, waligundua kuwa Yonathani na kijana aliyembebea silaha walikuwa hawapo.

18. Shauli akamwambia kuhani Ahiya, “Lilete hapa sanduku la Mungu.” (Wakati huo sanduku la agano la Mungu lilikuwa pamoja na Waisraeli.)

19. Shauli alipokuwa anaongea bado na kuhani, ghasia kambini kwa Wafilisti ziliongezeka zaidi na zaidi. Kwa hiyo Shauli akamwambia kuhani, “Acha; usililete tena sanduku la agano.”

20. Hivyo, Shauli na watu wake wakajipanga na kuingia vitani dhidi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walianza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe kwa mvurugiko mkubwa.

21. Waebrania waliokuwa upande wa Wafilisti, na waliokwenda nao huko kambini, wakageuka na kujiunga na Waisraeli waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani.

1 Samueli 14