Yeremia 5:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Manabii si kitu, ni upepo tu;maana neno lake Mungu halimo ndani yao.”Basi hayo na yawapate wao wenyewe!

14. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:“Kwa kuwa wao wamesema jambo hilo,sasa nitayafanya maneno niliyokupa wewe Yeremia kuwa moto.Watu hawa watakuwa kuni,na moto huo utawateketeza.

15. “Nami Mwenyezi-Mungu nasema juu yenu enyi Waisraeli:Mimi naleta taifa moja kutoka mbali,lije kuwashambulia.Taifa ambalo halishindiki,taifa ambalo ni la zamani,ambalo lugha yake hamuifahamu,wala hamwezi kuelewa wasemacho.

16. Mishale yao husambaza kifo;wote ni mashujaa wa vita.

17. Watayala mazao yenu na chakula chenu;watawamaliza watoto wenu wa kike na wa kiume.Watachinja makundi yenu ya kondoo na ng'ombe;wataiharibu mizabibu yenu na mitini yenu.Miji yenu ya ngome mnayoitegemea,wataiharibu kwa silaha zao.

18. “Lakini, hata katika siku hizo mimi Mwenyezi-Mungu nasema, sitawaangamiza na kuwamaliza kabisa.

19. Na watu wenu watakapouliza ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametutendea mambo hayo yote?’ Wewe utawaambia, ‘Nyinyi mlimwacha Mwenyezi-Mungu, mkaitumikia miungu ya kigeni katika nchi yenu. Basi ndivyo mtakavyowatumikia watu wengine katika nchi isiyo yenu.’

20. “Watangazie wazawa wa Yakobo,waambie watu wa Yuda hivi:

21. Sikilizeni enyi wajinga na wapumbavu;watu mlio na macho, lakini hamwoni,mlio na masikio, lakini hamsikii.

22. Mbona hamniogopi? Nauliza mimi Mwenyezi-Mungu!Kwa nini hamtetemeki mbele yangu?Mimi niliweka mchanga uwe mpaka wa bahari,kizuizi cha daima ambacho bahari haiwezi kuvuka.Ingawa mawimbi yanaupiga, hayawezi kuupita;ingawa yananguruma, hayawezi kuuruka.

23. Lakini watu hawa wana moyo wa ukaidi na uasi;wameniacha wakaenda zao.

24. Wala hawasemi mioyoni mwao;‘Na tumche Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,anayetujalia mvua kwa wakati wake,anayetupatia mvua za masika na mvua za vuli;na kutupa majira maalumu ya mavuno.’

Yeremia 5