4. Yeremia akawajibu, “Vema; nimesikia. Nitamwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyonisihi; jibu lolote atakalonipa Mwenyezi-Mungu, nitawaambieni; sitawaficha chochote.”
5. Kisha, watu wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi-Mungu na awe shahidi wa kweli na mwaminifu dhidi yetu ikiwa hatutafanya jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakavyokuagiza utuambie.
6. Iwe ni jambo la kupendeza au la, sisi tutaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu ambaye tunakutuma kwake ili tufanikiwe tutakapomtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.”
7. Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia.
8. Basi, Yeremia akamwita Yohanani mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, akawaambia,
9. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli ambaye mlinituma kwake nipeleke maombi yenu, asema hivi:
10. Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda.
11. Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake.
12. Nitawahurumieni na kumfanya mfalme awahurumie na kuwaacha nchini mwenu.
13. “Lakini mkisema: ‘Hatutaki kubaki katika nchi hii,’ na hivyo mkaacha kutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
14. na kusema kwamba mtakwenda kukaa nchini Misri, ambako hamtaona vita wala kusikia sauti ya tarumbeta wala kukosa chakula,
15. basi, sikilizeni asemavyo Mwenyezi-Mungu enyi mabaki ya Yuda. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama mmekusudia kuingia nchini Misri na kukaa huko,
16. basi, vita mnavyoviogopa vitawakumba hukohuko Misri, na njaa mnayoihofia itawaandama vikali hadi Misri, na mtafia hukohuko.
17. Watu wote wenye nia ya kwenda kukaa Misri watakufa kwa njaa na maradhi mabaya wala hakuna hata mmoja wao atakayebaki au kunusurika kutokana na maafa nitakayowaletea.