7. Lakini Ebedmeleki, towashi Mwethiopia aliyekuwa akifanya kazi katika ikulu, alipata habari kwamba walikuwa wamemtumbukiza Yeremia kisimani. Wakati huo mfalme alikuwa anabarizi penye lango la Benyamini.
8. Basi, Ebedmeleki akamwendea mfalme, akamwambia,
9. “Bwana wangu mfalme, watu hawa wamefanya kitu kibaya. Wamemtumbukiza yule nabii Yeremia kisimani ambamo kwa kweli atakufa kwa njaa, kwa maana hamna chakula tena mjini.”
10. Hapo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mwethiopia: “Chukua watu watatu kutoka hapa uende ukamtoe nabii Yeremia kisimani, kabla hajafa.”
11. Basi, Ebedmeleki akawachukua watu hao na kwenda pamoja nao ikulu kwa mfalme, wakaingia katika ghala ya ikulu; Ebedmeleki akatwaa nguo zilizotumika na matambara makuukuu, akamteremshia Yeremia kisimani kwa kamba.
12. Kisha Ebedmeleki, Mwethiopia, akamwambia Yeremia, “Weka hayo matambara kwapani mwako, kisha pitisha kamba hizo chini ya matambara hayo.” Yeremia akafanya hivyo.
13. Kisha wakamvuta Yeremia kwa kamba, wakamtoa kisimani. Baada ya hayo, Yeremia akaendelea kukaa katika ukumbi wa walinzi.
14. Wakati fulani mfalme Sedekia alitaka kumwona nabii Yeremia. Basi, akaagiza Yeremia aletwe kwenye mlango wa tatu wa hekalu la Mwenyezi-Mungu. Huko, mfalme alimwambia Yeremia, “Nataka kukuuliza jambo fulani; usinifiche kitu chochote.”
15. Yeremia akamjibu Sedekia, “Je, nikikuambia ukweli hutaniua? Na kama nikikushauri, hutanisikiliza.”
16. Hapo, mfalme Sedekia alimwapia Yeremia kwa siri akisema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu aliyetupa uhai, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa hawa wanaotaka kukuua.”
17. Hapo Yeremia akamwambia Sedekia: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama ukijitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, utayaokoa maisha yako na mji hautateketezwa kwa moto; nawe pamoja na jamaa yako mtaendelea kuishi.
18. Lakini usipojitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, basi, mji huu utatekwa na Wakaldayo nao watauteketeza kwa moto, nawe hutaweza kujiepusha mikononi mwao.”
19. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Nawaogopa Wayahudi waliokimbilia kwa Wakaldayo. Huenda nikakabidhiwa kwao, wakanitesa.”
20. Yeremia akamjibu, “Hutakabidhiwa kwao. Wewe sasa tii anachosema Mwenyezi-Mungu, kama ninavyokuambia, na mambo yote yatakuendea vema, na maisha yako yatasalimika.