Yeremia 2:22-28 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Hata ukijiosha kwa magadi,na kutumia sabuni nyingi,madoa ya uovu wako bado yatabaki mbele yangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

23. “Unawezaje kusema, ‘Mimi si najisi;sijawafuata Mabaali?’Tazama ulivyotenda dhambi kule bondeni;angalia ulivyofanya huko!Wewe ni kama mtamba wa ngamia,akimbiaye huko na huko;

24. kama pundamwitu aliyezoea jangwani.Katika tamaa yake hunusanusa upepo;nani awezaye kuizuia hamu yake?Amtakaye hana haja ya kujisumbua;wakati wake ufikapo watampata tu.

25. Israeli, usiichakaze miguu yakowala usilikaushe koo lako.Lakini wewe wasema: ‘Hakuna tumaini lolote.Nimeipenda miungu ya kigeni,hiyo ndiyo nitakayoifuata.’

26. “Kama vile mwizi aonavyo aibu akishikwa,ndivyo Waisraeli watakavyoona aibu;wao wenyewe, wafalme wao, wakuu wao,makuhani wao na manabii wao.

27. Hao huuambia mti: ‘Wewe u baba yangu,’na jiwe: ‘Wewe ndiwe uliyenizaa;’kwa maana wamenipa kisogo,wala hawakunielekezea nyuso zao.Lakini wakati wa shida husema: ‘Inuka utuokoe!’

28. “Lakini iko wapi miungu yako uliyojifanyia?Iinuke basi, kama inaweza kukusaidia,wakati unapokuwa katika shida.Ee Yuda, idadi ya miungu yakoni sawa na idadi ya miji yako!

Yeremia 2