Mwanzo 25:11-24 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu alimbariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akawa anaishi karibu na kisima cha Beer-lahai-roi.

12. Hawa ndio wazawa wa Ishmaeli mwanawe Abrahamu ambaye Hagari Mmisri, aliyekuwa mjakazi wa Sara, alimzalia Abrahamu.

13. Hii ni orodha yao kufuatana na kuzaliwa kwao: Nebayothi, mzaliwa wa kwanza, Kedari, Adbeeli, Mibsamu,

14. Mishma, Duma, Masa,

15. Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema.

16. Hao ndio watoto wa kiume wa Ishmaeli, waliokuwa asili ya makabila kumi na mawili; makazi na vijiji vyao vilijulikana kwa majina yao.

17. Ishmaeli alikuwa na umri wa miaka 137 alipofariki, akajiunga na wazee wake waliotangulia.

18. Wazawa wa Ishmaeli walikaa katika eneo lililo kati ya Hawila na Shuri, mashariki ya Misri, kuelekea Ashuru. Walikaa kwa utengano na wazawa wengine wa Abrahamu.

19. Hawa ndio wazawa wa Isaka mwana wa Abrahamu.

20. Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu. Rebeka alikuwa dada yake Labani.

21. Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba.

22. Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka, naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu.

23. Mwenyezi-Mungu akamwambia,“Mataifa mawili yamo tumboni mwako;makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana.Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine;mkubwa atamtumikia mdogo.”

24. Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha.

Mwanzo 25