Mathayo 13:8-24 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: Nyingine punje mia, nyingine sitini na nyingine thelathini.

9. Mwenye masikio na asikie!”

10. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

11. Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa.

12. Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

13. Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi.

14. Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya:‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa.Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

15. Maana akili za watu hawa zimepumbaa,wameyaziba masikio yao,wameyafumba macho yao.La sivyo, wangeona kwa macho yao,wangesikia kwa masikio yao,wangeelewa kwa akili zao,na kunigeukia, asema Bwana,nami ningewaponya.’

16. “Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia.

17. Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.

18. “Basi, nyinyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi.

19. Yeyote asikiaye neno juu ya ufalme wa Mungu bila kuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake.

20. Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na mara akalipokea kwa furaha.

21. Lakini halishiki na mizizi ndani yake; huendelea kulizingatia neno hilo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya neno hilo, anakata tamaa mara.

22. Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali hulisonga neno hilo, naye hazai matunda.

23. Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na kuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini.”

24. Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

Mathayo 13