Mathayo 13:20-35 Biblia Habari Njema (BHN)

20. Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na mara akalipokea kwa furaha.

21. Lakini halishiki na mizizi ndani yake; huendelea kulizingatia neno hilo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya neno hilo, anakata tamaa mara.

22. Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali hulisonga neno hilo, naye hazai matunda.

23. Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na kuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini.”

24. Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

25. Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake.

26. Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.

27. Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’

28. Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayangoe?’

29. Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia.

30. Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’”

31. Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake.

32. Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikisha ota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”

33. Yesu akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga madebe mawili na nusu, hata unga wote ukaumuka.”

34. Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano,

35. ili jambo lililonenwa na nabii litimie:“Nitasema nao kwa mifano;nitafichua yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.”

Mathayo 13