Kumbukumbu La Sheria 15:3-17 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Mnaweza kuwadai wageni, lakini madeni yote ya ndugu zenu wenyewe mtayafuta.

4. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika nchi anayowapa iwe mali yenu. Hakuna hata mmoja atakayekuwa maskini kati yenu,

5. mradi tu mumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kufuata kwa uangalifu amri ninazowapeni hivi leo.

6. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki kama vile alivyowaahidi. Nanyi mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. Kadhalika mtatawala mataifa mengi, lakini mataifa hayo hayatawatawala nyinyi.

7. “Kukiwa na maskini wa jamaa yenu katika miji ya nchi ambayo Mwenyezi-Mungu atawapa, msiwe wachoyo na wagumu kwake.

8. Badala yake, fumbueni mikono yenu na kumkopesha kwa hiari kiasi cha kutosha mahitaji yake.

9. Angalieni wazo ovu lisiwaingie mioyoni mwenu, mkasema: ‘Mwaka wa saba, mwaka wa kusamehe wadeni, uko karibu’; mkamfikiria ndugu yenu maskini kwa ukali na kukataa kumpa chochote; yeye aweza kumlilia Mwenyezi-Mungu dhidi yenu na hiyo ikawa dhambi kwenu.

10. Mpeni ndugu maskini kwa ukarimu bila kunungunika; maana kwa ajili ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki katika kazi zenu zote na katika kila mfanyalo.

11. Maana maskini hawatakosekana nchini; hivyo nawaamuru, muwe wakarimu kwa ndugu zenu wahitaji na maskini nchini mwenu.

12. “Kama nduguyo Mwebrania, mwanamume au mwanamke, akiuzwa kwako, atakutumikia kwa miaka sita, lakini katika mwaka wa saba, utamwacha huru.

13. Nawe utakapomwacha huru, usimwache aende mikono mitupu.

14. Mpe kwa ukarimu kile ambacho Mwenyezi-Mungu amekubariki: Kondoo, nafaka na divai.

15. Kumbukeni kwamba nyinyi mlikuwa watumwa huko Misri na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwakomboa; ndiyo maana leo nawaamuru hivyo.

16. Lakini akikuambia, ‘Sitaondoka kwako,’ kwa sababu anakupenda wewe na jamaa yako na anaridhika kuishi nawe,

17. basi, utachukua shazia na kutoboa sikio lake mpaka hiyo shazia iingie mlangoni naye atakuwa mtumwa wako milele. Kadhalika mtendee vivyo hivyo mtumwa wako wa kike.

Kumbukumbu La Sheria 15