Kumbukumbu La Sheria 10:12-22 Biblia Habari Njema (BHN)

12. “Sasa, enyi Waisraeli, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anataka nini kwenu, ila kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote, kumpenda, kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote,

13. na kuzitii amri na masharti ya Mwenyezi-Mungu ninayowawekea leo, kwa manufaa yenu wenyewe?

14. Tazama, mbingu hata mbingu za mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; dunia na vyote vilivyomo ni mali yake.

15. Tena Mwenyezi-Mungu aliwapenda babu zenu kwa dhati, akawachagua nyinyi wazawa wao kuwa watu wake badala ya watu wengine wote, kama ilivyo hivi leo.

16. Kwa hiyo, takaseni mioyo yenu, msiwe wakaidi tena.

17. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana. Yeye ni Mungu mkuu na mwenye nguvu, na wa kuogofya; hapendelei wala hapokei rushwa.

18. Huwapa haki yatima na wajane; huwapenda wageni na kuwapa chakula na nguo.

19. Basi, wapendeni wageni kwa kuwa nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri.

20. Mcheni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mtumikieni; ambataneni naye na kuapa kwa jina lake.

21. Yeye ni fahari yenu; ndiye Mungu wenu ambaye amewatendea haya mambo makubwa na ya kutisha mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe.

22. Babu zenu walipokwenda Misri, walikuwa watu sabini tu, lakini sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni.

Kumbukumbu La Sheria 10