22. “Kisha nyote mlikuja karibu nami mkaniambia, ‘Tutume watu watutangulie, waipeleleze nchi, halafu warudi kutujulisha njia bora ya kufuata na miji ipi tutaikuta huko.’
23. Jambo hilo lilionekana kuwa jema kwangu, nikawateua watu kumi na wawili, mtu mmoja kutoka katika kila kabila.
24. Watu hao walikwenda katika nchi ile ya milima, wakafika kwenye bonde la Eshkoli na kulipeleleza.
25. Waliporudi, walituletea baadhi ya matunda ya nchi hiyo na wakatuarifu kwamba nchi hiyo anayotupatia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni nzuri.
26. “Lakini nyinyi hamkufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kukataa kwenda katika nchi hiyo.
27. Mlinungunika ndani ya mahema yenu mkisema, ‘Mwenyezi-Mungu anatuchukia na ndiyo maana alitutoa nchini Misri. Alitaka kututia mikononi mwa Waamori, atuangamize.
28. Kwa nini tuende huko hali tumevunjika moyo kwa hofu? Wametuambia kuwa watu wa huko ni wakubwa na warefu kuliko sisi, na kwamba miji yao ni mikubwa na yenye kuta zifikazo mawinguni. Tena wamesema kwamba waliwaona wale wazawa wa Anaki!’
29. “Lakini mimi niliwaambieni hivi: ‘Msiwe na hofu wala msiwaogope watu hao.’
30. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambaye huwatangulia, yeye mwenyewe atapigana kwa ajili yenu kama alivyofanya mbele yenu kule Misri na
31. kule jangwani ambako mliona jinsi alivyowabeba safari hiyo yote kama vile baba amchukuavyo mwanawe mpaka mkafika hapa.
32. Lakini japo nilisema hayo yote, nyinyi hamkumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
33. ambaye aliwatangulia njiani na kuwatafutia mahali pa kupiga kambi zenu. Usiku aliwatangulieni kwa moto na mchana kwa wingu, ili kuwaonesha njia.
34. “Mwenyezi-Mungu aliyasikia manunguniko yenu, akakasirika, akaapa akisema:
35. ‘Hakuna hata mmoja wenu katika kizazi hiki kiovu atakayeingia katika nchi ile nzuri niliyoahidi kuwapa wazee wenu.
36. Kalebu mwana wa Yefune, ndiye tu atakayeiona; nami nitampatia nchi hiyo aliyoikanyaga iwe yake yeye na wazawa wake kwa kuwa amekuwa mwaminifu kabisa kwangu.’
37. Mwenyezi-Mungu alinikasirikia mimi pia kwa sababu yenu, akasema, ‘Hata wewe Mose hutaingia katika nchi hiyo.
38. Lakini msaidizi wako Yoshua mwana wa Nuni, ataingia humo. Basi, mtie moyo kwani yeye atawaongoza watu wa Israeli waimiliki nchi hiyo’.
39. Kisha Mwenyezi-Mungu akatuambia sisi sote, ‘Hao watoto wenu mnaoogopa kwamba watakuwa nyara za adui zenu, naam hao walio wadogo ambao hawajui bado kupambanua kati ya mema na mabaya, hao ndio watakaoingia huko, nami nitawapa wao nchi hiyo iwe yao.
40. Lakini nyinyi, geukeni na kurudi jangwani kuelekea Bahari ya Shamu.’
41. “Kisha mkanijibu, ‘Sisi tumemtendea dhambi Mwenyezi-Mungu, lakini sasa tutakwenda na kupigana kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru’. Hivyo, kila mmoja wenu akajitayarisha kupigana vita; maana mlifikiri kwamba lingekuwa jambo rahisi kuivamia nchi hiyo ya milima.