Hesabu 14:34-45 Biblia Habari Njema (BHN)

34. Kutokana na makosa yenu, mtataabika kwa muda wa miaka arubaini, sawa na zile siku arubaini mlizopeleleza ile nchi, mwaka mmoja kwa kila siku moja; mtatambua kwamba mimi nimechukizwa.

35. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema: Hakika nitawatenda hivyo nyinyi nyote mliokusanyika hapa kunipinga. Wote wataishia humuhumu jangwani na ni humu watakamofia.”

36. Wale watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza ile nchi waliorudi na kusababisha watu wamnungunikie Mwenyezi-Mungu kwa kuleta taarifa mbaya dhidi ya nchi,

37. watu hao waliotoa taarifa ya uovu kuhusu hiyo nchi, walikufa kwa pigo mbele ya Mwenyezi-Mungu.

38. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, walibaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi.

39. Naye Mose aliwaambia Waisraeli wote nao walilia kwa uchungu mwingi.

40. Kesho yake, waliamka alfajiri na mapema wakaenda sehemu za milimani, wakisema, “Sasa tuko tayari kabisa kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alituahidi. Tunakiri kwamba tulitenda dhambi.”

41. Lakini Mose akasema, “Sasa mbona mnavunja agizo la Mwenyezi-Mungu? Hivyo hamtafaulu!

42. Msiende huko milimani msije mkapigwa bure na adui zenu, maana, Mwenyezi-Mungu hayuko pamoja nanyi.

43. Mkiwakabili Waamaleki na Wakanaani, mtafia vitani; kwa kuwa mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu, yeye hatakuwa pamoja nanyi.”

44. Hata hivyo, wao walisisitiza kwenda juu milimani, ingawa sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wala Mose hakuondoka kambini.

45. Ndipo Waamaleki na Wakanaani, waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo ya milima, wakashuka, wakawashambulia na kuwashinda. Wakawafukuza mpaka mji wa Horma.

Hesabu 14