13. Siku hiyo, hofu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu itawakumba watu, na kila mtu atamshambulia mwenzake.
14. Watu wa Yuda watapigana kuulinda mji wa Yerusalemu; utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka nchi ya Yuda utakusanywa: Watakusanya dhahabu, fedha na mavazi kwa wingi sana.
15. Maafa makubwa yatawakumba farasi, nyumbu, ngamia, punda na wanyama wote watakaokuwamo katika kambi hizo za maadui.
16. Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda.
17. Iwapo taifa lolote duniani halitakwenda Yerusalemu kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, basi, mvua haitanyesha katika nchi yao.
18. Iwapo Wamisri watakataa kuiadhimisha sikukuu ya vibanda, basi, Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa ugonjwa uleule atakaowapiga nao mataifa yote yanayokataa kuiadhimisha sikukuu hiyo.
19. Hiyo itakuwa ndiyo adhabu itakayolipata taifa la Misri pamoja na mataifa yote yasiyoadhimisha sikukuu ya vibanda.
20. Wakati huo, kwenye njuga za farasi yataandikwa maandishi haya: “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu Vyungu vilivyomo katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu.
21. Kila chungu katika mji wa Yerusalemu na nchi ya Yuda kitawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili wote wanaotoa tambiko waweze kuvichukua na kuchemshia nyama ya tambiko. Wakati huo, hakutakuwapo mfanya biashara yeyote katika hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi.