Yeremia 52:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, mkazi wa mji wa Liba.

2. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama mabaya yote aliyotenda Yehoyakimu.

3. Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia sana watu wa Yerusalemu na Yuda hata akawafukuza mbali naye.Sedekia alimwasi mfalme wa Babuloni.

4. Ikawa katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, mwaka wa tisa wa kutawala kwake Sedekia, Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alifika na jeshi lake lote kuushambulia Yerusalemu, wakauzingira kila upande.

5. Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia.

6. Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwa na chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake.

7. Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari walikimbia wakatoka nje ya mji wakati wa usiku wakipitia njia ya lango katikati ya kuta mbili, kwenye bustani ya mfalme, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji wote. Waisraeli walikimbia kuelekea bonde la mto Yordani.

8. Lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia mfalme na kumteka katika tambarare za Yeriko, jeshi lake lote likatawanyika na kumwacha.

9. Basi Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni, huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu.

10. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda.

11. Kisha aliyangoa macho ya Sedekia na kumfunga pingu, akamchukua Sedekia Babuloni na kumtia kizuizini mpaka siku alipokufa.

12. Katika siku ya kumi ya mwezi wa tano, mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme ambaye alimtumikia mfalme wa Babuloni, aliingia Yerusalemu.

Yeremia 52