Yeremia 40:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Makapteni wote wa majeshi kutoka bara pamoja na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babuloni alikuwa amemtawaza Gedalia mwana wa Ahikamu, kuwa mkuu wa nchi, na kwamba alikuwa amemkabidhi wanaume, wanawake na watoto, yaani watu mafukara kabisa katika nchi ambao hawakuchukuliwa uhamishoni Babuloni,

8. walimwendea Gedalia huko Mizpa. Watu hao walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai kutoka Netofa, na Yezania mwana wa Maakathi; wote waliandamana na watu wao.

9. Gedalia aliapa mbele yao na mbele ya majeshi yao akisema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni nchini mumtumikie mfalme wa Babuloni, na mambo yote yatawaendea vema.

10. Mimi nitakaa Mizpa niwawakilishe nyinyi kwa Wakaldayo watakaofika kwetu; lakini nyinyi kusanyeni na kuhifadhi divai, matunda ya kiangazi na mafuta, mkae katika miji mnayoimiliki.”

11. Pia watu wa Yuda waliokuwa nchini Moabu na miongoni mwa Waamoni na nchini Edomu na nchi nyingine, waliposikia kwamba mfalme wa Babuloni alikuwa amewaruhusu watu wa Yuda wengine kubaki Yuda na kwamba alikuwa amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, kuwa mtawala wao,

12. wote walirudi kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyika na kwenda katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mizpa. Walichuma zabibu na matunda ya kiangazi kwa wingi sana.

Yeremia 40