Yeremia 26:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, katika nchi ya Yuda, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yeremia hivi:

2. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Simama katika ukumbi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, uwatangazie watu wa miji yote ya Yuda wanaofika kuabudu katika nyumba ya Mungu, mambo yote niliyokuamuru uwaambie, bila kuacha hata neno moja.

3. Labda watasikiliza na kuacha njia zao mbaya. Wakifanya hivyo, huenda nikabadili nia yangu kuhusu maafa niliyonuia kuwaletea kwa sababu ya matendo yao maovu.

4. “Utawaambia hivi: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Msiponisikiliza na kufuata sheria zangu nilizowawekea,

5. na msipoyajali wanayosema watumishi wangu manabii ambao nimekuwa nikiwatuma kwenu kila mara, ingawa hamkuwajali,

6. basi, nitaiharibu nyumba hii kama nilivyoharibu ile ya Shilo, na nitaufanya mji huu kuwa laana kwa mataifa yote ya dunia.”

7. Makuhani, manabii na watu wote walimsikia Yeremia akisema maneno haya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

8. Basi Yeremia alipomaliza kutangaza mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwamuru ayatangaze kwa watu wote, makuhani, manabii na watu wote walimkamata na kusema, “Utakufa!

9. Kwa nini umetabiri kwa jina la Mwenyezi-Mungu na kusema, nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa, bila wakazi?” Watu wote wakamzingira Yeremia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

10. Basi, wakuu wa Yuda waliposikia mambo hayo, walipanda kutoka katika nyumba ya mfalme, wakaenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaketi penye Lango Jipya.

Yeremia 26