Yeremia 2:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

2. “Nenda ukawatangazie waziwazi wakazi wote wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Naukumbuka uaminifu wako ulipokuwa kijana,jinsi ulivyonipenda kama mchumba wako,ulivyonifuata jangwanikwenye nchi ambayo haikupandwa kitu.

3. Israeli, wewe ulikuwa mtakatifu kwangu,ulikuwa matunda ya kwanza ya mavuno yangu.Wote waliokudhuru walikuwa na hatia,wakapatwa na maafa.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

4. Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi wazawa wa Yakobo. Sikilizeni enyi jamaa zote za wazawa wa Israeli.

5. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Wazee wenu waliona kosa gani kwanguhata wakanigeuka na kuniacha,wakakimbilia miungu duni,hata nao wakawa watu duni?

6. Hawakujiuliza:‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu aliyetutoa nchini Misri,aliyetuongoza nyikanikatika nchi ya jangwa na makorongo,nchi kame na yenye giza nene,nchi isiyopitiwa na mtu yeyote,wala kukaliwa na binadamu?’

7. Niliwaleta katika nchi yenye rutuba,muyafurahie mazao yake na mema yake mengine.Lakini mlipofika tu mliichafua nchi yangu,mkaifanya chukizo nchi niliyowapa iwe yenu.

8. Nao makuhani hawakujiuliza: ‘Yuko wapi Mwenyezi-Mungu?’Wataalamu wa sheria hawakunijua,viongozi wa watu waliniasi;manabii nao walitabiri kwa jina la Baalina kuabudu sanamu zisizo na faida yoyote.”

9. Mwenyezi-Mungu asema,“Kwa hiyo, mimi nitawalaumu nyinyi,na nitawalaumu wazawa wenu.

10. Haya, vukeni bahari hadi Kupro mkaone,au tumeni watu huko Kedari wakachunguze,kama jambo kama hili limewahi kutokea:

11. Kwamba kuna taifa lililowahi kubadilisha miungu yakeingawa miungu hiyo si miungu!Lakini watu wangu wameniacha mimi, utukufu wao,wakafuata miungu isiyofaa kitu.

12. Shangaeni enyi mbingu, juu ya jambo hili,mkastaajabu na kufadhaika kabisa.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

13. Maana, watu wangu wametenda maovu mawili;wameniacha mimi niliye chemchemi ya maji ya uhai,wakajichimbia visima vyao wenyewe,visima vyenye nyufa, visivyoweza kuhifadhi maji.

Yeremia 2