Walawi 4:5-23 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Huyo kuhani, aliyepakwa mafuta atachukua kiasi cha damu na kuingia nayo ndani ya hema la mkutano.

6. Atachovya kidole chake katika damu hiyo na kuirashia mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu upande wa mbele wa pazia la mahali patakatifu.

7. Kuhani atachukua sehemu ya damu na kuzipaka pembe za madhabahu ya kufukizia ubani wa harufu nzuri, mbele ya Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyoko karibu na mlango wa hema la mkutano.

8. Kisha atayaondoa mafuta yote ya ng'ombe huyo: Mafuta yanayofunika matumbo,

9. figo mbili na mafuta yaliyo juu yake na yale yaliyo kiunoni, na yale yaliyoshikamana na figo na ini; hizi ni sehemu zilezile zinazoondolewa kwa mnyama wa sadaka ya amani.

10. Kuhani atazichukua na kuziteketeza juu ya madhabahu ya kuteketezea sadaka.

11. Lakini ngozi ya huyo ng'ombe, nyama, kichwa, miguu, matumbo na mavi yake,

12. yaani ng'ombe mzima aliyesalia atampeleka na kumteketeza nje ya kambi mahali safi ambapo majivu hutupwa, naye atamchoma kwa moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo mahali pa kumwagia majivu.

13. “Iwapo jumuiya yote nzima ya Israeli imetenda dhambi bila ya kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu

14. mara dhambi hiyo itakapojulikana, jumuiya yote itatoa fahali mchanga awe sadaka ya kuondoa dhambi. Watamleta kwenye hema la mkutano.

15. Wazee wa jumuiya ya watu wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali, kisha atachinjwa mbele ya Mwenyezi-Mungu.

16. Yule kuhani aliyeteuliwa rasmi kwa kupakwa mafuta ataleta sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya hema la mkutano.

17. Atachovya kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza mbele ya pazia mara saba, mbele ya Mwenyezi-Mungu.

18. Kisha, sehemu ya damu atazipaka pembe za madhabahu iliyoko katika hema la mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyo karibu na mlango wa hema la mkutano.

19. Mafuta yote ya mnyama huyo atayachukua na kuyateketeza kwenye madhabahu.

20. Kwa hiyo atamfanya fahali huyu kama alivyomfanya yule mwingine wa sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, huyo kuhani atawafanyia watu ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, nao watasamehewa.

21. Kisha atamchukua fahali huyu na kumpeleka nje ya kambi na kumteketeza kwa moto kama alivyomfanya yule mwingine. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi ya jumuiya.

22. “Ikiwa mtawala ametenda dhambi bila kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, na hivyo akawa na hatia,

23. mara akijulishwa dhambi hiyo aliyotenda, ataleta sadaka yake ya beberu asiye na dosari.

Walawi 4