Walawi 20:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Kama mwanamume yeyote akilala na mnyama ni lazima auawe; na mnyama huyo lazima auawe.

16. Kama mwanamke akimkaribia mnyama na kulala naye ni lazima mwanamke huyo auawe na mnyama huyo pia; damu yao itakuwa juu yao wenyewe.

17. “Kama mwanamume yeyote akimwoa dada yake, binti ya baba yake au mama yake, na binti huyo akakubaliana na mwanamume huyo ambaye ni kaka yake, na kulala naye, hilo ni chukizo, ni lazima watengwe na rika lao kwani wamefanya jambo la aibu. Ni lazima mwanamume huyo awajibike kwa uovu wake.

18. Kama mwanamume akilala na mwanamke aliye mwezini, wote wawili ni lazima watengwe na watu wao; huyo mwanamume amelala na mwanamke aliye na hedhi, na huyo mwanamke amelala na mwanamume akiwa na hedhi.

19. Usilale na dada ya mama yako wala na shangazi yako, maana hao ni jamaa yako wa karibu. Wote watendao hayo watawajibika kwa uovu wao.

20. Kama mtu akilala na mke wa baba yake, mkubwa au mdogo, anamwaibisha baba yake mkubwa au mdogo; wote wawili watawajibika kwa dhambi yao; wote wawili watakufa bila watoto.

21. Kama mwanamume akimwoa mke wa ndugu yake, anamwaibisha ndugu yake, huo ni unajisi; wote wawili watakufa bila watoto.

22. “Mnapaswa kushika na kutekeleza masharti na maagizo yangu yote; la sivyo nchi ile ambamo ninawapeleka itawatapika.

23. Msizifuate desturi za taifa ninalolifukuza mbele yenu; kwani waliyafanya hayo yote, nami nikawachukia sana.

24. Lakini, nimekwisha waambia, ‘Mtarithi nchi yao, mimi nawapa nchi hiyo muimiliki, nchi inayotiririka maziwa na asali.’ Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu niliyewatenga na mataifa mengine.

25. Kwa hiyo, ni lazima mtofautishe kati ya mnyama asiye najisi na aliye najisi, kati ya ndege asiye najisi na aliye najisi. Msijifanye kuwa najisi kwa kugusa mnyama au ndege au chochote kitambaacho duniani ambacho nimekitenga kuwa ni najisi.

26. Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni mtakatifu, nami nimewatenga nyinyi na mataifa mengine ili muwe mali yangu, mtakuwa watakatifu.

27. “Mwanamume au mwanamke yeyote aliye mlozi au mchawi, ni lazima auawe kwa kupigwa mawe. Wote watawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe.”

Walawi 20