Walawi 20:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

2. “Waambie Waisraeli hivi: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli au mgeni anayekaa miongoni mwenu, akimtoa sadaka mtoto wake yeyote kwa mungu Moleki ni lazima mtu huyo auawe. Wananchi wa hapo watamuua kwa kumpiga mawe.

3. Mimi mwenyewe nitamkabili mtu huyo na kumtenga na watu wake kwa sababu alimtoa mmoja wa watoto wake sadaka kwa mungu Moleki na hivyo kupachafua mahali pangu patakatifu na jina langu takatifu.

4. Kama wananchi wa mahali hapo hawatamwadhibu mtu huyo kwa kumuua,

5. mimi mwenyewe nitamkabili mtu huyo na jamaa yake. Nitawatenga kutoka watu wao, yeye mwenyewe pamoja na wote waliokosa uaminifu kwangu kwa kumwendea mungu Moleki.

6. “Kama mtu yeyote anawaendea waaguzi wa mizimu na wachawi na hivyo kukosa uaminifu kwangu, nitamkabili mtu huyo na kumtenga na watu wake.

7. Kwa hiyo, jiwekeni wakfu muwe watakatifu; kwani mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

8. Shikeni masharti yangu na kuyatekeleza. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa.

9. Mtu yeyote amlaaniye baba yake au mama yake, ni lazima auawe. Amemlaani baba au mama yake, kwa hiyo damu yake itakuwa juu yake.

10. “Kama mwanamume akizini na mke wa jirani yake, ni lazima wote wawili wauawe.

11. Mwanamume akilala na mmoja wa wake za baba yake, anamwaibisha baba yake; wote wawili ni lazima wauawe. Damu yao itakuwa juu yao wenyewe.

12. Mwanamume yeyote akilala na mke wa mwanawe, wote wawili ni lazima wauawe. Wamefanya zinaa ya maharimu; wanawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe.

13. Kama mwanamume yeyote akilala na mwanamume mwenzake kana kwamba ni mwanamke, basi, wote wawili ni lazima wauawe kwani wamefanya jambo lililo chukizo; watawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe.

14. Kama mwanamume akioa mke na pia kumwoa mama yake, huo ni uovu; wote watatu ni lazima wateketezwe kwa moto kwani wamefanya uovu. Mtafanya hivyo ili uovu usiwe miongoni mwenu.

Walawi 20