Walawi 19:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

2. “Iambie jumuiya yote ya watu wa Israeli hivi: Ni lazima muwe watakatifu kwani mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mtakatifu.

3. Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

4. Msizigeukie sanamu za miungu, wala msijitengenezee sanamu za kusubu za miungu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

5. “Mnaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za amani, mtanitolea kama itakiwavyo ili mpate kukubaliwa.

6. Sadaka hiyo ni lazima iliwe siku hiyohiyo inapotolewa au kesho yake. Chochote kinachobaki hadi siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto.

7. Kama sehemu ya nyama yake italiwa siku ya tatu, tendo hilo ni chukizo; na sadaka hiyo haitakubaliwa,

8. naye atakayekula nyama hiyo ni lazima awajibike kwa uovu wake kwa sababu amekitia unajisi kitu kitakatifu cha Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo atatengwa na watu wake.

9. “Utakapovuna mavuno ya nchi yako, usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba wala usirudi nyuma kukusanya mabaki.

10. Msirudie kukusanya kila kitu katika shamba la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini; utawaachia maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

11. “Msiibe, msidanganye wala kuambiana uongo.

12. Msiape uongo kwa jina langu hata kulikufuru jina la Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

13. “Usimdhulumu jirani yako wala kumwibia. Mshahara wa mtu aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi.

Walawi 19