1. Mwenyezi-Mungu alizungumza na Mose, baada ya wana wawili wa Aroni kufa wakati ule walipomkaribia.
2. Alimwambia, “Mwambie ndugu yako Aroni asiingie mahali patakatifu nyuma ya pazia wakati usiokubaliwa. Asiingie mahali hapo kwani ndipo nitakapotokea katika wingu juu ya kiti cha rehema. Asipotii, atakufa.
3. Aroni ataingia mahali patakatifu sana akiwa na fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
4. Ataoga mwili wote katika maji, kisha atavaa mavazi matakatifu. Ataingia mahali hapo akiwa amevaa mavazi matakatifu: Joho la kitani baada ya nguo ya ndani ya suruali ya kitani na akiwa amevaa kanzu ya kitani na kujifunga mkanda wa kitani.
5. Atatwaa kutoka jumuiya ya watu wa Israeli beberu wawili kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
6. “Aroni atamtoa huyo fahali sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na jamaa yake.
7. Kisha, wale beberu wawili atawaweka kwenye mlango wa hema la mkutano.
8. Atawapigia kura hao beberu wawili, kura moja kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na nyingine kwa ajili ya Azazeli.
9. Atamleta yule beberu ambaye kura ilimtaka kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kumtolea sadaka ya kuondoa dhambi.
10. Lakini yule beberu aliyetakiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atatolewa mbele ya Mwenyezi-Mungu akiwa hai ili kufanya ibada ya upatanisho kuhani atamwacha aende jangwani kwa Azazeli, ili kuondoa dhambi za jumuiya.
11. “Aroni atamtoa fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya jamaa yake, kisha atamchinja fahali huyo sadaka ya kuondoa dhambi.
12. Halafu atachukua chetezo na kutwaa makaa madhabahuni mbele ya Mwenyezi-Mungu na ubani konzi mbili uliosagwa vizuri sana.
13. Ili asije akafa, atauleta ubani huo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuutia katika moto ili moshi wa ubani huo ukifunike kifuniko cha sanduku la agano.
14. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na kunyunyiza kwa kidole chake upande wa mashariki juu ya kiti cha rehema kisha atainyunyizia mbele ya sanduku la agano mara saba kwa kidole chake.
15. “Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele.
16. Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi.
17. Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje.