11. Kuhani atakayemtakasa mtu huyo atamleta mbele ya Mwenyezi-Mungu karibu na mlango wa hema la mkutano pamoja na vitu alivyoleta.
12. Kuhani atachukua mwanakondoo dume mmoja na kumtolea sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita. Atafanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu.
13. Kisha atamchinja huyo mwanakondoo katika mahali patakatifu, wanapochinjia wanyama wa sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa. Sadaka hii ya kuondoa hatia, kama ilivyo sadaka ya kuondoa dhambi, ni mali yake kuhani; ni sadaka takatifu kabisa.
14. Kuhani atachukua kiasi cha damu ya sadaka ya kuondoa hatia na kumpaka mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia.
15. Kisha, kuhani atachukua kiasi cha ile theluthi moja ya mafuta na kuyatia katika kiganja cha mkono wake wa kushoto.
16. Atachovya kidole cha mkono wake wa kulia katika mafuta hayo na kumnyunyizia huyo mtu anayetakaswa mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu.
17. Kiasi cha mafuta yanayobaki katika kiganja chake atampaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
18. Yale mafuta yaliyobaki atampaka huyo mtu kichwani. Hivyo kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.
19. Kuhani atatolea sadaka ya kuondoa dhambi na kumfanyia huyo mtu anayetakaswa ibada ya upatanisho ili kumwondolea unajisi wake. Kisha atamchinja mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.
20. Kuhani atatolea ile sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka juu ya madhabahu. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi.
21. “Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini, hana uwezo wa kutoa vitu hivyo, basi ataleta mwanakondoo dume mmoja kuwa fidia ya sadaka ya kuondoa hatia ambaye atafanyiwa ishara ya kutoa sadaka ili kumfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho. Ataleta pia kilo moja ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka na mafuta theluthi moja ya lita.
22. Ataleta pia hua wawili au makinda mawili ya njiwa kadiri anavyoweza mmoja atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
23. Siku ya nane atamletea kuhani vitu hivyo mbele ya mlango wa hema la mkutano kwa ajili ya utakaso wake mbele ya Mwenyezi-Mungu.
24. Kuhani atamchukua huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita na kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu.
25. Atamchinja huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia. Kuhani atachukua kiasi cha damu na kumpaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia.
26. Kuhani atatia kiasi cha mafuta hayo katika kiganja cha mkono wake wa kushoto.
27. Kisha atamnyunyizia huyo mtu kwa kidole chake cha kulia kiasi cha hayo mafuta yaliyomo katika kiganja chake cha kushoto mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu.