36. Hata hivyo, kisima au chemchemi ya maji vitakuwa safi. Lakini chochote kinachogusa mzoga kitakuwa najisi.
37. Iwapo sehemu ya mzoga inaziangukia mbegu za kupanda, mbegu hizo hazitakuwa najisi.
38. Lakini ikiwa mbegu zimetiwa katika maji ili kuota na sehemu yoyote ya mzoga ikaziangukia, basi, mbegu hizo ni najisi kwenu.
39. “Iwapo mnyama yeyote mnayeruhusiwa kula, anakufa mwenyewe, yeyote atakayegusa mzoga wake, atakuwa najisi mpaka jioni.
40. Mtu yeyote akila nyama ya mzoga huo atafua mavazi yake na atakuwa najisi mpaka jioni. Na yeyote atakayebeba mzoga huo, atafua mavazi yake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
41. “Kiumbe chochote kitambaacho duniani ni najisi kwenu, kamwe msikile.
42. Chochote kiendacho kwa tumbo lake, chochote kiendacho kwa miguu yote minne au nyayo nyingi, naam, chochote kitambaacho, kamwe msikile kwa maana ni najisi kwenu.
43. Hivyo msije mkawa najisi kwa kula viumbe vitambaavyo na hivyo mkawa najisi.
44. Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi Mungu wenu, jiwekeni wakfu na kuwa watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu.
45. Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu; kwa hiyo muwe watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu.”
46. Hiyo basi, ndiyo sheria kuhusu wanyama, ndege na viumbe vyote hai ambavyo huishi majini na nchi kavu,
47. ili kupambanua kati ya kisicho najisi na kilicho najisi; kinachoweza kuliwa na kisichoweza kuliwa.