13. Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani.
14. Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani.
15. Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: Kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea.
16. Yeye hakufanywa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho.
17. Maana Maandiko yasema: “Wewe ni kuhani milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.”
18. Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu.
19. Maana sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu.
20. Zaidi ya hayo, hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo.
21. Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia:“Bwana ameapa,wala hatabadili nia yake:‘Wewe ni kuhani milele.’”
22. Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
23. Tena: Hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao.
24. Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake.
25. Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu.